MAMLAKA YA KUZUIA RUSHWA NA UHUJUMU UCHUMI ZANZIBAR
ZANZIBAR ANTI-CORRUPTION AND ECONOMIC CRIMES AUTHORITY
KUPINGA VITENDO VYA RUSHWA KWENYE UCHAGUZI HULETA MATOKEO CHANYA
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Hassan Abdalla Mitawi amefikishwa mahakamani kwa makosa kadhaa ikiwemo kosa la matumizi mabaya ya ofisi na ukwepaji kodi.
Mkurugenzi huyo alipanda kizimbani mnamo tarehe 17/12/2014 majira ya saa 5 asubuhi katika mahakama ya mkoa Vuga, mbele ya Hakimu Ali Ameir.
Akisoma mashitaka mbele ya hakimu huyo, Muendesha mashtaka Abdalla Issa Mgongo, alisema mshitakiwa huyo amefikishwa mbele ya mahakama hiyo akiwa na mashitaka mawili.
Alisema kosa la kwanza linalomkabili ni kukwepa kulipa kodi kinyume na kifungu cha 44 kifungu kidogo cha (1)(e) na kifungu kidogo cha (2) pamoja na kifungu cha 61 vya sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar.
Katika kosa hilo la kwanza mshtakiwa Hassan Abdalla Mitawi na Mamy James Matata kwa nyakati tofauti mwaka 2014 katika jengo la Shirika la Habari na Utangazaji (ZBC ) Televisheni kwa makusudi walifanya biashara ya kuuza magari bila ya kujiandikisha kuwa walipa kodi na kulipa kodi hizo kwa mamlaka husika.
Aidha Mgongo alisema kosa la pili la matumizi mabaya ya ofisi kinyume na vifungu vya 53 na 61 vya sheria namba moja ya mwaka 2012 ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar.
Katika kosa la pili muendesha mashitaka huyo alisema kwamba mshtakiwa kwa nyakati tofauti mwaka 2014 katika jengo la ZBC Televisheni akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la ZBC alitumia nafasi yake kwa kufanya biashara ya kuuza magari katika eneo la ofisi kwa lengo la kujipatia maslahi binafsi.
Kwa upande wake Hakimu Ali Ameir alimtaka mshtakiwa huyo kutojibu lolote mahakamani hapo kwa sababu ni kesi inayosikilizwa na Mahakama Kuu, hivyo ataenda kujibu shitaka hilo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu.
Hata hivyo, mshitakiwa amepewa dhamana ya maandishi ya shilingi milioni moja pamoja na wadhamini wawili kwa kima hicho hicho kwa kila mmoja na kesi hiyo kuahirishwa hadi tarehe 14/01/2015.